Jumamosi, 23 Januari 2016

Eleza kwa mifano, dhima za fasihi namna zinavyofungamanishwa na mazingira ya mwandishi wa kazi ya Fasihi na jamii yake kwa ujumla.



Kwa mujibu wa Mulokozi, (1996) anaeleza dhana ya fasihi kwa upana kuwa, huko ulaya dhana hii imekuwa ikihusishwa na neno la Kilatini “Literra” ambalo lina maana ya “herufi “au “uandikaji”. Neno la Kiingereza “Literature” limechipuka kutokana na neno hilo la kilatini.
Wamitila, ( 2013:3) anaifafanua  fasihi kwa maana finyu na pana, Anasema  kuwa  katika ufafanuzi wa fasihi kuna utata   wa neno  lenyewe fasihi. Aghalabu,  tunapoitumia maana hii huwa tunajenga maana yake finyu kurejelea utanzu kama mashairi, tamthiliya , riwaya  na hadithi fupi. Katika maana yake pana anasema kuwa ni jumla ya   insha fulani, hotuba, matini , vibonzo au katuni na hata filamu.
Stella,( 2015: 17) anasema Fasihi ni taaluma ya sanaa ya lugha, yenye ubunifu ndani yake,  na inayo  fikisha ujumbe kwa hadhira  kwa kutumia njia ya maandishi au kwa njia ya  mdomo.
Kwa mtazamo wangu ,  nawezakusema kuwa  Fasihi ni  ujuzi wa kutumia  sanaaa ya lugha iliyobuniwa kwa lengo la kufikisha ujumbe  kwa hadhira kwa kutumia njia ya maaandishi au njia ya mdomo.
Ni kweli dhima ya fasihi hujifungamanisha na mazingira ya mwandishi lakini si kwa mazingira ya mwandishi pekee, bali kwa jamii nzima itakayofikiwa na kazi husika. Hivyo basi, kwa muktadha huo tutangalia  ni kwa jinsi gani dhima za  fasihi hujifungamanisha na mazingira  kama ifuatavyo;
Kuelimisha, kazi ya fasihi hulenga kuelimisha jamii kwani dhana ya kuelimisha ndiyo chachu ya maendeleo katika jamii, hasa katika kujikomboa kutoka chini ya utawala wa ukandamizaji na utawala wa kinyonyaji au usiofaa. Mfano; katika tamthiliya ya “Kivuli Kinaishi” ya Mohammed, (1990: 128) anasema;
Sauti Nyingi; ( kutoka nje ambako zinajongea ndani)  “Sisi ni vizazi vipya vya Giningi, vizazi vya walioangamia,,,Ni vizazi vya walio didimia, Sisi  sasa tuna kinywa kipana, tunauwezo   wa kuamua tunavyotaka,,,, kuamua wenyewe,,, kwa masrahi ya sote,,, hatutachagizwa tena na uchawi, tunakuja ,,,tunakuja.”                                                                      
Dhima ya kifalsafa, huelezea vipengele mbalimbali kuhusu maisha ya watu katika jamii. Waandishi husema kuwa palipo  na mvutano wa wema na ubaya  lazima wema ushinde, hivyo haki hutendeka . Dhana hii inajidhihirisha katika jamii yeyote ile, kwani kila jamii inahitaji haki, ili iweze kujenga jamii yenye usawa na demokrasia. Dhana  hii imejitokeza katika tamthiliya ya Kivuli Kinaishi ya Mohammed, (1990:128)  ambapo, mwandishi ananukuliwa akisema,
Macho ya Bi Kirembwe; ( sauti ya macho inaonekana inatoka mbali); Mimi ni shahidi wa maovu yote uliyoyatenda  ya kudidimiza  na kuangamiza.(Bi Kirembwe kwa kuchechemea);Hata macho yangu leo yanasema.
Dhima ya kiitikadi, Hii ni dhima ambayo inategemea muktadha wa jamii husika, nafasi ya mtunzi na msimamo wakewe kulingana na matatizo na migogoro ya wakati wake katika jamii husika. Mzingira (Mandhari), mwandishi huchukua kazi yake katika mazingira yanayo mzunguka au jamii iliyo mzunguka  kwa ujumla wake, kulingana na ujumbe alioukusudia kwa jamii yake. Mfano; Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii”ya Marium Ba, (1994:103) anasema ;
“Kwa maoni yangu, uvaaji wa suruali ulikuwa unatisha, kama mtu hukuwa na unene uliozidi ka ma ule wa kina mama wa kimagharibi.”  
Dhima ya kiuchumi, uchumi ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji mali, na kuongeza kipato  kupitia shughuli za kiuchumi na kijamii. Uchumi wa jamii hukua endapo kama kutakuwepo na uongozi bora katika jamii, yaani unapinga rushwa na unyonyaji. Katika tamthiliya ya “Kivuli Kinaishi” mwandishi amejadili kwa upana katika (Uk; 24- 25) kwa kumtumia mhusika; Bawabu II ambaye anapokea rushwa kutoka kwa mfanya biashara, kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kinaondoa usawa katika jamii ya Giningi.
Dhima ya kisiasa, dhamira hii inadokezwa na waandishi wengi, kwani ni suala ambalo huwezi kulitenga na maisha ya mwandishi na jamii yake kwa ujumla, Kwa mfano; harakati hisi za kisiasa wakati wa ukoloni, zilikuwepo kwasababu  rasilimali nyingi ziliibiwa na wakoloni kwa ajili ya kuimarisha miradi yao, ilihali,  viwanda vidogo vidogo vya Waafrika vikididimizwa na wakoloni hawa. Mwandishi wa “Barua Ndefu kama hii” katika (Uk; 25) anasema;
“Je ilikuwa sawa kwetu sisi kufurahia  utelekezwaji wa viwanda vidogo vidogo vya uhunzi, ufundi wowote ule na ushonaji viatu?”
Dhima ya utamaduni, katika utamaduni;  fasihi inamajukumu ambayo ni pamoja na  kuhifadhi na kurithisha amali za jamii, kuburudisha ,kuhasa, na kulekebisha jamii. Kazi yeyote ya fasihi uhusishwa moja kwa moja na  utamaduni, kwani  mwandishi huchota maudhui( dhamira) yake kwa kuzingatia dhana ya utamaduni wa jamii husika, iliyomzunguka na tamaduni zingine za ki- ulimwengu katika kuonesha uhalisia wa kile kinachoelezwa na mwandishi.  Kwa mfano;  Katika Tamthiliya ya “Kivuli Kinaishi” mwandishi ameonesha mambo ya kiutamaduni  kama vile Matumizi Ya Ngoma, Kuwalisha unga wa Ndere na unga wa rutuba. Mwandishi ametumia Ngoma za ki-utamaduni katika (UK. 48) Anasema;
“Ngoma inasikika tena kwa mpigo mmoja mmoja, pole pole na taratibu na wote ispokuwa wazee wanacheza na halafu  gafla inasita”
Hivyo basi, Fasihi inajifungamanisha na jamii yake lakini sio tu mazingira ya mwandishi pekee, bali kwa kuangalia  mazingira kwa ujumla wake kijiografia na kiutamaduni.





                                                     






                                 MAREJELEO
Marium Ba, (1994) Barua Ndefu Kama hii. Mkuki na Nyota publisher. Dar es Salam
Mulokozi, M .M (1996) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
Mohammed, S (1990) Kivuli Kinaishi. Oxford University Press; East Africa Ltd: Kenya.
Stella, F (2015) Fasihi ya Kiswahili, Ushairi, Tamthiliya, na Riwaya. KiberaSeaboys General Interprises.Dodoma.

Maoni 3 :